
Afisa Habari wa Klabu ya Simba Hajji Manara amesema, ili kusiwe na mashaka katika ligi kuu TFF wanatakiwa kuhakikisha itakapofika mzunguko wa 20 wa Ligi kuu Klabu zote ziwe zimecheza sawa kwani Azam FC watakuwa na michezo ya akiba ambayo Simba haitakubali.
Manara amesema, Azam FC imeshiriki katika uvunjifu wa kanuni kwa kuacha ligi ikiendelea na kwenda kushiriki mashindano ambayo yapo nje ya ratiba.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Bodi ya Ligi Kuu Boniface Wambura amesema, Bodi inapokea malalamiko yote na hata maoni pia, na hata Azam FC kwenda nchini Zambia ni ruhusa kwa ajili ya maandalizi ya mashindano ya Afrika.
Wambura amesema, malalamiko kwa vilabu mbalimbali hususani vilabu ambavyo vinafukuzana katika msimamo wa ligi kuu ni fikra ambazo wanahisi Azam FC kwenda Zambia anapendelewa kwenye ratiba suala ambalo sio kweli.
Wambura amesema, vilabu vinaangalia kuwa Azam FC kwenda Zambia inazidi kujinoa zaidi hivyo ligi kuwa ngumu kwa wapinzani wa Azam FC suala ambalo sio kweli bali ni ruhusa ambayo hata misimu iliyopita Azam FC ilishiriki pia mashindano hayo.