Tuesday , 13th Dec , 2016

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa – TAKUKURU imewafikisha katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, maafisa wawili pamoja na kibarua mmoja wa Mamlaka ya Mapato nchini TRA kwa makosa matatu ya kuomba na kupokea rushwa.

 

Wakili wa TAKUKURU Bw. Lupyana Mwakatobe ameiambia mahakama hiyo kuwa katika kosa la kwanza lililofanyikia Desemba 18 mwaka huu, wakiwa watumishi wa Mamlaka ya Mapato TRA kituo cha Kariakoo, watuhumiwa hao Bw. Liberatus Retentius Rugumisa na Bw. Kenneth Emmanuel Mawere waliomba rushwa ya shilingi milioni hamsini kutoka kwa mfanyabiashara wa duka la kubadilishia pesa Bw. Humphrey Lema, kwa lengo la kumpunguzia makadirio ya kodi ya ongezeko la thamani VAT ambayo mfanyabiashara huyo alipaswa kulipa.

Wakili huyo ameendelea kudai kuwa Desemba 23 mwaka huu, watuhumiwa hao walitenda kosa la pili kwa kupokea pesa za Tanzania shilingi milioni kumi ikiwa ni sehemu malipo ya rushwa ya shilingi milioni hamsini waliyoiomba katika kosa la kwanza na kwamba pesa hizo walizipokea katika duka la kubadilishia pesa liitwalo Cate Bureau De Change lililopo Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Aidha katika kosa la tatu, Wakili Mwakatobe amedai kuwa mshtakiwa namba moja na namba mbili wakishirikiana na mshtakiwa namba tatu aliyejulikana kwa jina la Nassoro Saidi Nassoro ambaye ni kibarua katika ofisi hiyo ya TRA, walipokea dola za Marekani 2744 kutoka kwa mfanyabiashara huyo huyo kinyume na sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa.

Watuhumiwa hao wamesomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala Bw. Adelf Sachore, ambapo mtuhumiwa namba mbili Bw. Kenneth Emmanuel Mawere yupo nje kwa dhamana wakati watuhumiwa namba moja na namba tatu wamerudishwa mahabusu hadi kesi yao itakapotajwa tena Desemba 27 mwaka huu.