Thursday , 12th Dec , 2019

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack, amekiri kuwepo kwa baadhi ya wanawake mkoani kwake kuogeshwa dawa ili kuvutia wanaume katika mahusiano, huku akitangaza kufanya ukaguzi wa Ndoa zinazofanyika mkoani humo kwa ajili ya kuzuia ndoa za utotoni hasa kwa wanafunzi.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack.

RC Telack ameyabainisha hayo leo Desemba 12, 2019, wakati akizungumza na kipindi cha Supa Breakfast cha East Africa Radio, kinachoruka kila siku ya Jumatatu hadi Ijumaa, kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa 4 asubuhi.

"Ni kweli kuna watoto wanaogeshwa dawa, hii ni mila potofu ila niseme tunachopambania kwa sasa ni kuhakikisha tunamaliza suala la utoro shuleni, na  tumewaonya wazazi yeyote ambaye atajihusisha na vitendo visivyo halali kwa mtoto wa kike, atachukuliwa hatua za kisheria" amesema Telack.

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa ameongeza kuwa "Ndoa zote zinazofungwa kwenye Mkoa tunapeleka watu kujua nani anaolewa, kwa sababu kulikuwa na ongezeko la mimba za wanafunzi na walipoona hivyo wakaamua kubadilisha jina kutoka Ndoa na kuita mzunguko kwa hiyo tunahakikisha tunapeleka watu wetu kwenye hizo sherehe"