Wednesday , 18th Mar , 2020

Mlinzi wa klabu ya Highlands Park ya nchini Afrika Kusini na timu ya taifa ya Tanzania, Abdi Banda amezungumzia tetesi kuhusu kukumbwa na virusi vya Corona.

Abdi Banda

Banda ametoa taarifa hiyo baada ya tetesi mbalimbali kusambaa katika mitandao ya kijamii zikimuhusisha mlinzi kukumbwa na virusi vya Corona na kupelekea kutengwa na timu yake ili aweze kurejea katika hali yake ya kawaida.

Kupitia mtandao wa Instagram, Banda amekanusha taarifa kuhusu kukubwa na virusi vya Corona, ambapo amesema, "napenda kutoa shukrani zangu kwa wote mlioguswa/shtushwa na habari juu yangu, kikubwa kila kitu kimeenda sawa".

"Kwa baraka za Mwenyezi Mungu imegundulika haukuwa ugonjwa unaosumbua kwa sasa duniani (virusi vya Corona). Ahsanteni sana MUNGU awabariki", ameongeza.

Abdi Banda aliitwa katika kikosi cha timu ya taifa Taifa Stars, kilichokuwa kikijiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu michuano ya AFCON dhidi ya Tunisia lakini hakuwasiri kambini, hali iliyozusha wasiwasi huo.

Hata hivyo mchezo huo uliahirishwa na Shirikisho la Soka barani Afrika CAF kutokana na tishio la kusambaa kwa virusi vya Corona.