Monday , 30th Mar , 2020

Afisa Habari wa Ruvu Shooting, Masau Bwire amesema kuwa endapo michezo itarejea na kuchezwa bila ya mashabiki haitoleta ladha nzuri kwa sababu mashabiki ndiyo wanaonogesha staili yao ya mpapaso.

Masau Bwire

Kauli hiyo imekuja kufuatia hivi karibuni Bodi ya Ligi (TPBL)kubainisha baadhi ya mapendekezo yake kwenye ligi ikiwemo kucheza mechi zilizobakia bila ya mashabiki pale itakaporuhusiwa kurejea tena.

Bwire amesema kuwa ni jambo la msingi ambalo limefanywa na Bodi ya Ligi kuzuia mashabiki ili kupambana na Virusi vya Corona ila haitapendeza kucheza mechi hizo zilizobakia bila ya mashabiki.

Siku zote nimekuwa nikisema kwamba Ruvu Shooting inacheza kama Barcelona, sasa kutokana na kuzuiwa kwa mashabiki kujitokeza uwanjani iwapo ligi itaanza tena, mpapaso hautapendeza sana bila mashabiki lakini ni lazima tuzingatie utaratibu", amesema Masau.

Tunaomba hili lipite na ligi irejee kwani hili jambo siyo la kuchukulia utani. Watanzania pia ni muhimu kuchukua tahadhari na Virusi vya Corona ili wawe salama,” ameongeza.

Serikali kupitia kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Machi 17 ilisimamisha shughuli zote zinazohusu mikusanyiko isiyo ya lazima ikiwa ni pamoja na Ligi Kuu Bara, Ligi Daraja la Kwanza, Ligi ya Wanawake ili kupisha maambukizi ya Virusi vya Corona.

Ruvu Shooting ipo nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 39 baada ya kucheza mechi 28 mpaka sasa.