Sunday , 12th Jul , 2020

Leo Julai 12 ni siku nyingine tena ambayo nchi itasimama kwa dakika 90 kupisha mtanange wa nguvu kati ya Simba na Yanga, awamu hii ikiwa ni katika Kombe la Shirikisho.

Simba na Yanga

Mchezo huu ni mkubwa si tu kutokana na uhasama wa timu hizi mbili, bali kwa jinsi kila timu inavyohitaji ushindi ili kufanikisha kitu fulani kikubwa katika historia yake. Yafuatayo ni mambo 5 ambayo unatakiwa kuyafahamu kuelekea mchezo huo.

Mosi: Mchezo huu ni wa tatu kuzikutanisha timu hizo msimu huu, mchezo wa kwanza uliochezwa Januari 4, 2020 ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2, mchezo wa pili uliochezwa Machi 8, 2020 ulimalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa bao moja kupitia kwa Bernard Morrison.

Pili: Mchezo huu hautakuwa na mashabiki wengi zaidi kama ilivyokuwa ikitokea katika michezo ya hapo nyuma kutokana na tahadhari ya janga la Corona, ambapo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limetangaza kuwa watazamaji watakaoruhusiwa ni 30,000 pekee.

Tatu: Simba inahitaji kushinda mechi hii ili kuhalalisha kile wanachokiamini kuwa hakuna raha ya kusheherekea ubingwa bila ya kuifunga Yanga, huku Yanga ikihitaji zaidi ushindi ili kuweka matumaini ya kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao (Kombe la Shirikisho barani Afrika).

Nne: Jumla ya waamuzi 6 watahusika katika kusimamia mchezo huo wa leo, kutokana na kuwepo kwa changamoto ya maamuzi katika michezo ya hivi karibuni, ambapo waamuzi wawili watawekwa mahususi kwenye magoli yote mawili.

Tano: Tahadhari kwa timu zote mbili kutokana na matokeo yatakayopatikana kwenye mchezo wa leo hasa Yanga, kuwa endapo watapoteza mchezo huu watapoteza nafasi ya kucheza michuano ya kimataifa msimu ujao hivyo kuhatarisha vibarua vya makocha hata baadhi ya wachezaji, kwani matukio kama hayo yaliwahi kujitokeza katika mechi mbalimbali huko nyuma ambazo makocha walifukuzwa baada ya kupoteza mchezo wa watani.