Saturday , 8th Aug , 2020

Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Kheri James amesema katika uchaguzi Mkuu wa mwaka huu wamejiandaa kufanya siasa safi kwa kuzingatia maadili na kanuni za uchaguzi huku wakiwasihi taasisi na asasi zingine kufanya vivo hivyo.

Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Kheri James

Akizungumza katika Mkutano wa baraza kuu la UVCCM linalofanyika jijini Dodoma amesema ni muhimu kulinda staha ya kila chama na wagombea ili umoja na mshikamano katika Nchi yetu uendelee.

“Sisi tunaapa mbele ya watanzania wote umoja wa vijana utakuwa wa kwanza kulinda na kuyaenzi  maadili ya uchaguzi na hivyo tunawasihi wenzetu kupitia taasisi na asasi zingine wafanye hivyo, wakifanya kinyume chake sisi tutailinda nchi yetu na tutakilinda chama chetu na viongozi  wetu’’- amesema James.

Mwenyekiti huyo amesema kuwa leo ni siku ya kihistoria kwao kama vijana baada ya kuaminiwa na Chama kwa mara nyingine na kupewa nafasi ya kutafuta wawakilishi wao katika vyombo vya maamuzi na kudai kuwa haki imerudi ili kupimwa kama vijana hao ni waadilifu.

Aidha amesema umoja wa Vijana wa UVCCM ndiyo tanuru la hoja na kwamba ndio msingi wa viongozi imara wa leo na kesho.