Saturday , 7th May , 2022

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ameiagiza Wizara Ujenzi pamoja na wataalam kukutana na idara ya kazi ya mkoa wa Mwanza ili kuchunguza kama kuna madai yoyote ya mishahara kwa wafanyakazi wanaojenga daraja la Kigongo Busisi maarufu kama daraja la JPM ili waweze kulipwa na ujenzi usisimame.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa daraja la JPM

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Mei 7, 2022 Jijini Mwanza mara baada ya kubaini upungufu wa wafanyakazi 200 katika ujenzi wa daraja hilo lenye urefu wa kilometa 3.2 ambalo limegharimu zaidi ya shilingi bilioni 600.

Ujenzi wa daraja la JPM unatekelezwa na kampuni ya kichina ya  CCECC ambayo pia inatekeleza ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR ambapo Waziri Mkuu Majaliwa ameitaka kampuni hiyo kuacha tabia ya kuwapa ajira wafanyakazi wa daraja kwenye ujenzi wa reli na badala yake wabaki kumalizia ujenzi wa daraja hilo.

Katika hatua nyingine Mbunge wa jimbo la Sengerema Hamis Tabasamu, amemueleza Waziri Mkuu kuwa malipo ya wafanyakazi hao ni madogo hali inayopelekea wengine kuamua kuondoka.