JPM ashtukia umaarufu wa Tanga kushuka

Jumanne , 20th Oct , 2020

Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), leo tarehe 20 Oktoba akiwa Korogwe Jijini  Tanga ameelezea wasi wasi wake juu ya kushuka kwa umaarufu wa Jiji la Tanga ambapo amebainisha mikakati ya kuinua hadhi ya Jiji hilo.

Pichani ni Dkt John Pombe Magufuli, Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM.

Miongoni mwa mikakati aliyoitaja kuwa itainua umaarufu na kurejesha hadhi ya Jiji la Tanga ni pamoja na kuiboresha reli ambayo tayari imeshaanza safari zake, upanuaji wa bandari ya Tanga, ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Ohima (Uganda) pamoja na uboreshwaji wa miundo mbinu ya barabara na upanuaji wa uwanja wa ndege ambao utaruhusu ndege kubwa kutua.

''Tanga ina historia kubwa katika taifa hili lakini Tanga ni miongoni mwa majiji ya mwanzo kabisa katika taifa la Tanzania lakini pia palikuwa na viwanda vingi watu walipata ajira nyingi, kila kitu ilikuwa Tanga baadae umaarufu wa Tanga ukashuka chini ndiyo maana katika awamu ya tano tumejipanga kufanya mabadiliko ya kweli katika Mkoa wa Tanga" Dkt. John Magufuli.

Aidha Magufuli aliongeza kuwa Jiji hilo litawekwa katika ramani ya kiuchumi katika miaka mitano ijayo '' Tunataka kuiweka hii Tanga iwe hub (kitovu) ya maendeleo''