Magufuli aeleza alivyomjengea barabara Msuya

Jumatano , 21st Oct , 2020

Katika muendelezo wa kampeni za urais Tanzania, mgombea wa Chama Cha Mapinduzi Dkt John Magufuli ameeleza sababu zilizofanya asimamie kikamilifu ujenzi wa Barabara ya kwenda kwa Waziri Mstaafu Cleopa Msuya wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro.

Mgombea wa Chama Cha Mapinduzi Dkt John Magufuli

Magufuli ameyaeleza hayo leo kwenye mkutano wa kampeni wilayani Mwanga, ambapo amesisitiza kuwa watu walimshangaa lakini ukweli kuwa anapoishi Msuya pia kuna watu wanaishi na barabara hiyo wanatumia wote hivyo ni maendeleo kwa wote.

''Nashukuru sana kwa mapokezi hapa Mwanga, huwezi kuitaja historia ya Mwanga bila kumtaja mzee Cleo[a Msuya, nikiwa waziri wa Ujenzi nilisimamia ujenzi wa barabara ya kwenda kwake, watu walihoji sana lakini historia yake kwenye taifa hili haiwezi kufutika'' - amesema Magufuli.

Aidha amemuonya mkandarasi anayejenga mradi wa maji katika wilaya za Mwanga na Same kwa kumtaka akamilishe haraka vinginevyo atamfukuza.

''Nimekuwa waziri wa Ujenzi najua makandarasi wanasimamiwaje, huu mradi wa maji hapa Mwanga naomba niwaambie sasa nitausimamia mwenyewe na nimemwambia mkandarasi ndani ya mwezi mmoja aniambie anaukamilishaje, asipofanya hivyo namfukuza hamtawaona tena'' ameongeza.

Pia ameahidi kuwajengea hospitali ya wilaya. ''Hapa Mwanga najua mna jambo lenu la ubaguzi mara hawa Wasangi na wale Wagweno lakini mimi najua sisi wote ni watanzania na kwasababu mnahitaji Hospitali nitawajengea Hospitali ya Wilaya hapa Mwanga na sio mbaya Usangi kuwa na hospitali ya wilaya na Mwanga mkawa nayo'', amesema Magufuli.