Vyama 9 Zanzibar vyatoa neno uteuzi wa Dkt. Mwinyi

Jumanne , 3rd Nov , 2020

Viongozi wa umoja wa vyama 9 vya upinzani Zanzibar, wamesema kuwa wameyakubali kwa asilimia 100 matokeo ya urais na watahakikisha wanamuunga mkono Rais Dkt. Hussein Mwinyi, ili kuleta maendeleo ya Wazanzibar.

Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu Taifa wa Chama cha Democrasia Makini, Ameir Hassan Ameir, ambaye alikuwa ni mgombea urais wa Zanzibar, kupitia chama hicho katika uchaguzi.

"Sisi vyama vyote 9 tumekubaliana na matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar na tunamuunga mkono kwa 100% Rais wa Zanzibar wa awamu ya 8, Dkt Mwinyi, na tuko tayari kushirikiana naye usiku na mchana kuhakikisha maendeleo ya Zanzibar yanapatikana", amesema Ameir.

Vyama hivyo ni UPDP, DP, UMD, CCK, TLP, NLD, SAU, NRA na Demokrasia Makini, ambapo pia kwa pamoja vimewasisitiza wakazi wa visiwani humo kushirikiana kwa pamoja ili kuijenga Zanzibar, huku wakisisitiza kuwa uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki.