Alhamisi , 6th Oct , 2022

Kampuni, taasisi na viwanda ambavyo havitoi mkataba kwa waajiriwa wataanza kuchukuliwa hatua baada ya Serikali kuanza kutangaza msako kwa waajiri.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi

Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea maadhimisho ya wiki ya vijana inayotarajia kuanza Oktoba 8, 2022.

Katambi amesema kwa muda mrefu wamekuwa wakihamasisha waajiri kutoa mikataba kwa wafanyakazi wao jambo ambalo utekelezaji wake umekuwa wa kusuasua katika baadhi ya maeneo.

"Kuna baadhi ya maeneo waajiriwa hawana mikataba, wengine wana mikataba ambayo haijaandikwa ukomo wake, linapotokea jambo wanaenda kujaza tarehe ya mwisho ya ukomo ili kumtoa muhusika katkka ajira jambo ambalo halikubaliki,"

Amebainisha kuwa kukosekana kwa mikataba imekuwa ikiweka ugumu kwa waajiriwa kudai haki zao pindi wanapoppteza ajira.Pia, amesema baadhi ya waajiri wanatoa mishahara iliyo chini ya kima cha chinj cha mshahara kilichowekwa na Serikali jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Katika hatua nyingine, Katambi amesema Katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2022, Serikali imeendelea kufanya kaguzi za utekelezaji wa sheria nchini ambapo jumla ya kaguzi 859 zimefanyika katika maeneo ya kazi na waajiri waliokiuka Sheria kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria.

Pia wizara imeendelea kuratibu ajira za wageni kwa kutoa vibali vya kazi ambapo 3,298 vimetolewa, makusanyo ya maduhuli yanayotokana na vibali vya kazi na leseni za wakala wa ajira vimefikia Sh8.69 bilioni.