Ijumaa , 6th Aug , 2021

Waziri wa Kilimo Mhe. Prof. Adolf Mkenda amesema ifikapo mwaka 2022 serikali haitota vibali vya kuagiza sukari nje ya nchi kwa wawekezaji kwani nchi itakuwa imeshafikia uwezo wakuzalisha sukari toshelevu nchini.

Waziri wa Kilimo Mhe. Prof. Adolf Mkenda

Prof. Mkenda amesema hayo Jijini Dodoma katika kongamano la saba la wadau wa sekta ya kilimo ambapo amebainisha kuwa upungufu wa sukari nchini unatokana na makampuni kushindwa kuongeza uchakataji wa miwa kutoka kwa wakulima na si uhaba wa miwa.

“Baada ya mwaka huu Serikali haitotoa vibali kwa wawekezaji waliopewa viwanda vya sukari kuagiza sukari nje kwani tayari watakuwa wamefikia uwezo wa kuzalisha sukari toshelevu ikiwa ni pamoja na kukamilika kwa uanzishwaji wa viwanda vipya vya sukari hapa nchini,” amesema Prof. Mkenda.

Pia Waziri Mkenda ameeleza kuwa zaidi ya tani 350,000 za miwa ya wakulima katika Bonde la Kilombero mkoani Morogoro zinateketezwa kwa moto kutokana na kukosa soko la uhakika huku zaidi ya tani 40,000 za sukari zinaagizwa kutoka nje ya nchi jambo ambalo sio sahihi kwani viwanda vya sukari vilivyopo nchini vinapaswa kuongeza uwezo wao ili kuimarisha soko la wakulima.

Hata hivyo Waziri Mkenda amesema kuwa mtu yeyote atakayeingiza sukari kiholela ni msaliti wa nchi hivyo atachukuliwa hatua kali za kisheria.