Alhamisi , 24th Nov , 2022

Zaidi ya wafanyabiashara 1000 wa matunda aina ya tikiti maji katika soko la Tazara Veternary jijini Dar es Salaam wamepewa muda wa hadi Januari mwakani 2023 kuondoka katika eneo hilo ili kupisha uendelezaji na uwekezaji kwa mmiliki husika wa eneo hilo.

Wafanyabiashara wa tikiti

Wakizungumza na EATV leo Novemba 24, 2022, wafanyabiashara hao wa tikiti wameonyesha kutoridhishwa kuondoka katika eneo hilo kwa kile walichodai kwamba soko hilo limekuwa ni soko kubwa katika nchi za Afrika Mashariki na na hivyo wameiomba serikali kuliangalia suala hilo kwa jicho la huruma

Akizungumzia hatua hiyo Makamu Mwenyekiti wa soko hilo Omari Mbwana, amesema atakayeathirika zaidi ni mfanyabiashara na mkulima kwa kuwa tikiti zinazolimwa nchi nzima zinaletwa katika soko hilo hivyo itawachukua muda kupata soko ambalo litazoeleka kama lilivyokuwa soko la Tazara veternary.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa idara ya viwanda, biashara na uwekezaji kutoka Manispaa ya Temeke Ramadhani Gurumukwa, amekiri kuwepo kwa taarifa za kutaka kuondolewa kwa wafanyabiashara hao na kwamba kwa sasa wameshaanza jitihada za  kuwapatia masoko mengine ambayo watatumia wafanyabiashara wa tikiti kufanya biashara zao za tikiti maji.