Jumatano , 14th Jan , 2015

Wakati Tanzania ikiwa katika nafasi ya nne kwa ulizalishaji wa zao la mahindi barani Afrika, imeelezwa kuwa watumiaji wa mahindi wanakula 30% ya sumu kuvu inayotokana na uhifadhi duni wa mahindi.

Utafiti uliofanywa na mradi wa USAID Tuboreshe Chakula umebaini kuwa kutokana na uhifadhi duni na mbinu bora za kilimo cha mazao ya nafaka kama mahindi, alizeti na maharage unasababisha ukungu kwenye mazao hayo  hali inayosababisha sumu kuvu yenye madhara makubwa kwa mlaji.

Madhara hayo ni pamoja na saratani ya ini,ambapo mmoja  wa watafiti wa sumu hiyo na mhadhiri Mwandamizi wa chuo kikuu cha sayansi cha Nelson Mandela, Dk. Martin Kimanya amesema sumu hiyo haiwezi kuondolewa kwa kupika chakula na badala yake watumiaji wanapaswa kuchagua nafaka kwa kuondoa zile ambazo zimebadilika rangi na kuwa na ukungu.

Kutokana na tatizo hilo mradi wa USAID tuboreshe chakula umeanza mikakati ya kuinusuru jamii ikiwemo kwa kutoa elimu kwa wasindikaji wa vyakula pamoja na wakulima ili kufahamu sumu kuvu na madhara yake.