Jumatano , 27th Jul , 2016

Mahakama kuu kanda ya Iringa imemuhukumu askari wa jeshi la polisi kikosi cha kutuliza ghasia mjini Iringa Pasificus Cleophace Simon miaka 15 jela kwa kosa la kumuua bila kukusudia aliyekuwa mwandishi wa habari na mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa

Nje ya jengo la mahakama kuu kanda ya Iringa

Mahakama kuu kanda ya Iringa imemuhukumu askari wa jeshi la polisi kikosi cha kutuliza ghasia mjini Iringa Pasificus Cleophace Simon miaka 15 jela kwa kosa la kumuua bila kukusudia aliyekuwa mwandishi wa habari na mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari mkoani Iringa Daud Mwangosi mnamo Sept 2, 2012.

Tarehe 25 mwezi wa saba mwaka huu mahakama hiyo ilimtia hatiani mtuhumiwa huyo kwa kosa la kuua bila kukusudia ambapo mapema hii leo Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa Dkt. Paul Kiwelo akisoma hukumu hiyo amesema mahakama imepitia mapendekezo ya kila upanda ili kujiridhisha ambapo amesema pamoja na kuwepo kwa maombi ya upande wa utetezi kuwa mtuhumiwa aachiliwe huru kutokana na kuwa na wategemezi 5 hoja hiyo haina uzito ukilinganisha na ukubwa wa kosa alilolifanya askari huyo.

Hata hivyo Jaji Kiwelo ameiambia mahakama kuwa kesi hiyo pamoja na kuwa na maslahi kwa jamii na familia ya marehemu kulikuwa na ombi la upande wa jamuhuri kuwa mtuhumiwa anapaswa kupewa adhabu ya kifungo cha maisha, amesema mahakama hiyo imeona imuhukumu miaka 15 ili iwe fundisho kwake na askari wengine.

Akizungumza nje ya mahakama hiyo wakili wa upande wa utetezi Lwezaura Kaijage amesema kutokana na kesi hiyo ilivyoendeshwa analo jukumu la kupitia upya ili kuona kama kuna ulazima wa kukata rufaa kuikataa adhabu hiyo.

Deogratus Nsokolo ni Rais wa Klub za wandishi wa habari Tanzania na Deodatus Balile ni makamu mwenyekiti jukwa la wahariri Tanzania wamesema pamoja na mahakama kutenda haki katika kesi hiyo lakini changamoto kubwa ipo kwa jeshi la polisi ambalo limekuwa likitumika kunyima uhuru kwa wanahabari kufanya kazi zao hali ambayo inadaiwa kuwa siyo ya kawaida.

Kwa upande wa ndugu wa marehemu wakiongozwa na mke wa marehemu Mama Itika Mwangosi, wamevipongeza vyombo vya habari kwa kulivalia njuga suala hilo, na kuwataka kuendeleza mapambano hayo kwa niaba ya wanyonge.

Aidha ndugu hao wamesema kesi ya msingi imekwisha, jambao ambalo halimaanishi kuwa wanaridhika na hukumu, bali wanajipanga kuanzisha kesi ya madai licha ya ukweli kwamba hata kama hukumu ingekuwaje, ndugu yao hawezi kurudi duniani.

Ni takribani miaka minne sasa imepita tangu auawe mwandishi na mwenyekiti wa klabu ya wandishi wa habari mkoani Iringa Daudi Mwangosi na kesi hiyo iliyojaa sura ya ubabe kutoka kwa jeshi la polisi kwa kuwazuia wanahabari kufanya kazi zao na kumficha mtuhumiwa huyo jambo lililowashangazo hata viongozi wa mahakama imehitimishwa hii leo.

Itika Mwangosi akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya hukumu