Jumanne , 24th Jan , 2023

Herbert Gappa (7), Mtoto anayesoma Darasa la Kwanza Shule ya Msingi ya Mchepuo wa Kiingereza iliyopo Mji wa Bariadi mkoani Simiyu, amelazwa hospitalini baada ya kudaiwa kupigwa na kujeruhiwa vibaya sehemu zake za mwili na baba yake mzazi, ambaye ni askari Polisi, Abati Benedicto Nkalango

Mtoto huyu anayetibiwa katika Hospitali ya Somanda Mjini Bariadi, amekatishwa masomo yake darasani baada ya baba yake kumtendea unyama huu, kinyume cha sheria za nchi na haki za binadamu.

Akizungumzia ukatili huu aliotendewa mtoto huyu wa kiume, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Somanda, Dk. Costantine Emmanuel, amesema madaktari na wauguzi wanaongeza jitihada za kunusuru uhai wa mtoto huyu, nguvu kazi ya Taifa.

Akizungumzia ukatili huu, Mwalimu Benadetha Katendege, anaposoma mtoto huyu, amesema wamegundua shambulio hilo la kudhuru mwili baada ya mtoto huyo kuonekana kukosa morari ya masomo darasani.

Kufuatia hali hiyo, Askari Polisi huyo anayetuhumiwa kutenda ukatili huo kwa mwanaye wa kumzaa, tayari yupo mikononi mwa Polisi, ambapo umma unasubiri kuona hatua gani zitachukuliwa dhidi yake.

Tanzania imesaini mkataba wa kimataifa wa kulinda haki za binadamu, hivyo ni muhimu ukatili huu ukadhibitiwa ili kujenga jamii inayoheshimiana