Jumanne , 27th Jan , 2015

Wanunuzi wa bidhaa mbalimbali katika soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam wamekutana na adha baada ya wafanyabiashara wenye maduka sokoni hapo kufunga maduka yao.

Wafanyabiashara hao wamefunga maduka kwa madai ya kuishinikiza polisi kuwaeleza mwenyekiti wao yuko wapi baada ya kukamatwa na polisi na baadaye kuelezwa kuwa hayupo kituoni.

Katika soko la Kariakoo ambalo limezoeleka kuwa na msongamano wa watu hali ilikuwa tofauti ambapo mitaa ilikuwa tulivu huku baadhi ya vijana na wafanyabiashara wakiwa wamekaa kwenye makundi nje ya maduka yao ambapo baadhi ya wanunuzi mbali na kulalamikia upotevu wa nauli wameitaka serikali kukaa pamoja na wafanyabiashara hao wakubaliane ili kuepusha migomo ya mara kwa mara inayofanywa na wafanyabiashara hao ambayo pia inaikosesha serikali mapato.

Kwa upande wa madereva wa magari ya mizigo ambao wanaegesha maeneo hayo ya Kariakoo wamesema mgomo huo unawaathiri kwa kiwango kikubwa kwani wenye magari wanahitaji hela ya siku lakini pia familia zao zinawategemea.

Akizungumzia suala hilo katibu mkuu jumuiya ya wafanyabiashara nchini Bw Silva Kiondo, amesema wao hawana mgomo isipokuwa wamelazimika kufunga maduka yao ili wakamtafute mwenyekiti wa jumuiya hiyo Bw Minja ambaye wamedai kuwa alikamatwa na polisi na kufikishwa kituo kikuu cha polisi lakini baadaye walipokwenda kwa ajili ya kumdhamini walipewa maelezo kuwa hayupo kapelekwa Dodoma.

Hata hivyo EATV ilifunga safari hadi kituo kikuu cha polisi ili kupata ufafanuzi zaidi lakini hali iliyokuwepo kituoni hapo ilikuwa tofauti na siku nyingine ambapo polisi walionekana kutanda eneo hilo huku wengine wakiwa na silaha za moto.

Polisi walikuwa wakizuia watu kuingia katika eneo hilo na kamanda wa polisi kanda maalum ya Dar es Salaam Suleiman Kova alipotafutwa kwa njia ya simu hakujibu badala yake alituma ujumbe mfupi kwa maandishi akidai kuwa yuko Dodoma kwenye mkutano.