Jumanne , 12th Aug , 2014

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii nchini Tanzania imetenga shilingi bilioni 1.8 kukabiliana na ugonjwa wa Ebola endapo utaingia nchini.

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii nchini Tanzania Dkt Seif Rashid.

Fedha hizo zimetengwa sambamba na mkakati unaoendelea wa kuwabaini watu wenye maambukizi ya virus vya ugonjwa huo katika mipaka ya nchi pamoja na viwanja vya ndege nchini.

Akiongea leo Jijini Dar es Salaam, Waziri wa wizara hiyo Dkt. Seif Rashid amesema wizara hiyo imeongeza kiwango cha ufuatiliaji katika maeneo hayo kwa kuwakagua abiria katika viwanja vya ndege vya kimataifa hapa nchini ambapo pia wizara imeagiza kifaa cha Thermoscaner kitakachosaidia kuwabaini wagonjwa wenye dalili za ugonjwa huo.

Dkt. Rashid amesema vifaa vya kujikinga na ugonjwa huo vipo vya kutosha kwa ajili ya matumizi kwa watoa huduma na tayari vimeanza kusambazwa kutoka Bohari ya Dawa MSD kwenda hospitali za wilaya, mikoa na rufaa nchini.

Katika hatua nyingine, Daktari bingwa wa upasuaji wa magonjwa ya ndani katika hospital ya rufaa ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam nchini Tanzania Dkt. Kariameli Wandi ameitahadharisha jamii dhidi ya ugonjwa wa homa ya ini ambao imeonekana kushika kasi hapa nchini huku wananchi wakishindwa kutambua dalili za ugonjwa huo mapema.

Akizungumza na Kurasa leo jijini Dar es Salaam Dkt. Wandi amesema hata matibabu ya ugonjwa wa homa ya ini yamekuwa ni changamoto kutokana na mgonjwa wa homa ya ini kulazimika kutumia dawa za kufubaza ugonjwa UKIMWI, ARVs.