Jumamosi , 16th Jan , 2016

Vikao vya kamati za Bunge la 11 vinataraji kuanza Januari 21 mwaka huu, huku ofisi ya Bunge ikiongeza kamati mbili na kuzifanyia marekebisho kamati nyingine.

Kamati ya Kanuni ya Bunge iliyoundwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Job Ndugai hivi karibuni, imekutana Jijini Dar es Salaam na kuridhia mapendekezo ya mabadiliko katika muundo wa kamati za Bunge yaliyowasilishwa na Spika ili kuendana na mabadiliko ya Muundo wa Wizara katika Serikali ya awamu ya Tano.

Mabadiliko hayo ambayo yamefanywa chini ya kanuni ya 155 (3) ya kanuni za Kudumu za Bunge yamezingatia madaraka aliyonayo Spika kufanya marekebisho kwenye nyongeza za kanuni kwa kushauriana na kamati hiyo.

Akizungumza na wajumbe wa kamati hiyo Mh. Ndugai ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati hiyo amesema amelazimika kufanya mabadiliko katika muundo wa kamati ili kuendana na mabadiliko ya Wizara na kwa kuzingatia kuwa muundo wa kamati umetajwa kwenye nyongeza ya nane.

Katika muundo huo Kamati mbili mpya zimeundwa ambazo ni kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na kamati ya kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma.

Akifafanua kuhusu maamuzi ya Kikao hicho, katibu wa Bunge Dkt. Thomas Kashililah amesema kikao hicho kimekuwa na mafanikio makubwa na kuridhia mapendekezo ya Mhe. Spika kama yalivyowasilishwa.

Aidha Dkt. Kashililah aliongeza na kusema kuwa Kamati nyingine zimefanyiwa mabadiliko kwenye majina na nyingine mbili kuunganishwa na kufanya kamati mpya za Bunge kuwa kama ifuatavyo:

Kamati zilizounganishwa ni:

• Kamati ya Huduma na maendeleo ya Jamii - imeunganishwa kutoka iliyokuwa Kamati ya Maendeleo ya Jamii na kamati ya Huduma za Jamii

• Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama – imeunganishwa kutoka iliyokuwa Kamati ya Ulinzi na Usalama na kamati ya mambo ya Nje. Kamati zilizofanyiwa Marekebisho madogo kwenye majina ni:

• Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira (awali ilikuwa Kamati ya Viwanda na Biashara)

• Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii (awali ilikuwa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira)

• Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa (awali ilikuwa Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa)

Kamati zilizobakia kama ilivyokuwa awali ni pamoja na:
• Kamati ya Uongozi,
• Kamati ya Kanuni za Bunge,
• Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge,
• Kamati ya Katiba na Sheria
• Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji,
• Kamati ya Miundombinu na
• Kamati ya Nishati na Madini.

Wabunge wote wanatakiwa kuwasili Dodoma tarehe 20 Januari, 2016 tayari kwa kuanza Vikao vya Kamati kabla ya Mkutano wa Bunge unaotarajiwa kuanza tarehe 26 Januari, 2016.