Jumatatu , 16th Nov , 2015

Matokeo ya ubunge jimbo la Lulindi: Jerome Bwanausi CCM kura 17,715 (87.3%), Modesta Makaidi NLD kura 1,638, Amina Mshamu CUF kura 714, Francis Ngaweje ACT kura 213

Aliyekuwa mgombea wa kiti cha ubunge katika jimbo la Lulindi kupitia CCM, Jerome Bwanausi ametangazwa kuwa mshindi wa kiti hicho baada ya kuwabwaga wenza watatu kutoka vyama vya NLD, CUF na ACT Wazalendo, katika uchaguzi mdogo uliofanyika jana.

Jerome ameshinda kiti hicho kwa kupata kura 17,715 sawa na asilimia 87.3, akifuatiwa na Modesta Makaidi wa chama cha NLD aliyepata kura 1,638, Amina Mshamu wa CUF akipata kura 714 na mgombea wa ACT Wazalendo Francis Ngaweje akiambulia kura 213.

Katika uchaguzi huo, idadi ndogo ya watu imejitokeza kupiga kura ambapo kati ya watu 59,027 walioandikishwa ni watu 20,580 pekee waliojitokeza sawa na asilimia 30.

Hali imekuwa tofauti na siku ya uchaguzi mkuu wa Rais na madiwani Oktoba 25 ambapo katika jimbo hilo watu zaidi ya 45,000 walijitokeza kupiga kura.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana jana kuhusu sababu za watu kutojitokeza kwa wingi, baadhi ya wakazi wa jimbo hilo lililoko wilayani Masasi walidai kutokuwa na taarifa za tarehe ya kupiga kura huku wengine hususani vijana wakidai kususia zoezi hilo kutokana na kukatishwa tama na matokeo ya uchaguzi mkuu.

Idadi kubwa ya watu waliojitokeza ni watu wazima wanaokadiriwa kuwa na umri wa kuanzia miaka 55 na kuendelea.

Uchaguzi huu mdogo umefanyika kufuatia kuahirishwa hapo awali kutokana na makosa yaliyokuwa katika karatasi za kupigia kura ambapo jina la mgombea wa CUF lilikosewa.

Kwa matokeo hayo, CCM imefanikiwa kuongeza kiti cha ubunge wa majimbo katika bunge la 11 kutoka viti 188 hadi viti 189.