Jumatano , 13th Jan , 2021

Mkuu wa wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo, amefanya ziara ya kushtukiza katika ofisi za TANESCO wilayani humo na kukutana na malalamiko lukuki toka kwa wananchi waliofika katika ofisi hizo wakidai kucheleweshewa kuwekewa umeme majumbani mwao ikiwemo kero ya kukatika katika kwa umeme.

Mkuu wa wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo,

Majira ya saa tatu asubuhi DC Jokate, alifika katika ofisi za TANESCO wilaya na kukutana na wananchi waliofika mahala hapo wakisubiri huduma na kupata fursa ya kusikiliza kero ya wananchi hao, huku wengi wao wakilalamikia hasara wanayoipata pindi umeme unapokatika.

Mara baada ya kusikiliza malalamiko ya wananchi hao na kujiridhisha, DC Jokate, akaagiza kuswekwa rumande kwa baadhi ya watendaji wa idara hiyo huku akiutaka uongozi kuhakikisha inatatua kero inayowakabili wananchi haraka iwezekanavyo.

Kwa upande wa viongozi wa TANESCO licha ya kukiri kuwepo kwa changamoto hizo lakini wakaahidi kuanza kuyafanyia kazi mapungufu hayo mara moja.