Jumatano , 7th Mei , 2014

Waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Gordon Brown ameisifu na kuipongeza Tanzania kwa kufanya vizuri katika bara la Afrika kwa uandikishaji watoto shule.

Rais Kikwete akiwa na waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Gordon Brown

Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu ya Kimataifa – UN Special Envoy for Global Education - na Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Mheshimiwa Gordon Brown amesema kuwa Tanzania imefanya vizuri zaidi kuliko nchi nyingine yoyote ya Afrika katika uandikishaji wa watoto kuanza shule.

Aidha, Mheshimiwa Brown amesema kuwa hana uhakika kama Watanzania wanajua fika kuwa nchi yao imefikia mafanikio makubwa mno ya elimu ambayo bado ni ndoto tu kwa nyingine nyingi za Afrika.

Kwa sababu hiyo na kwa sababu ya mafaniko hayo, Mheshimiwa Brown amesema kuwa Umoja wa Mataifa na taasisi zake na nyingine za kimataifa ziko tayari kuisaidia Tanzania kufikia lengo la kusajili watoto wote kwa asilimia 100 ya watoto wote wanaotakiwa kuingia shule katika muda wa uongozi wa Rais Kikwete na kabla hajaondoka madarakani mwishoni mwa mwaka ujao.

“Mheshimiwa Rais, tunapenda kukupongeza kwa kufanya vizuri sana katika nyanja ya elimu. Haya ni mafanikio ya uongozi wako. Umewezesha asilimia 98 ya watoto wanaotakiwa kuanza shule kuingia shule. Hakuna nchi nyingine ya Afrika ambayo imefikia mafanikio kiasi hiki. Tunapenda kukusaidia na kufanya kazi na wewe ili tufikie asilimia 100, “ amesema Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Uingereza katika mkutano na Rais Kikwete.

Rais Kikwete na Mheshimiwa Brown wamekutana kwenye Hoteli ya Hilton mjini Abuja ambako wote wawili wanakaa wakati wanahudhuria Kongamano la Uchumi Duniani – kwa Bara la Afrika lilioanza leo, Jumatano, Mei 7, 2014 katika mji mkuu wa Nigeria.

Ameongeza Mheshimiwa Brown, “Mheshimiwa Rais, sasa tunataka kusaidia kuwapeleka shule kiasi cha watoto 100,000 ambao ni asilimia mbili ambao kwa sasa hawaendi shule. Tunajua hawa ni watoto wa makabila ya wafugaji ambao wanahamahama kila siku na mifugo yao na watoto wao vile vile. Lakini Serikali yako imepiga hatua kubwa, kubwa kuliko inavyofikiriwa na mataifa mengine ya Afrika katika kukabiliana na hali hiyo.”

Mheshimiwa Gordon Brown pia amesema kuwa Umoja wa Mataifa na taasisi zake ziko tayari kuisaidia Tanzania katika kuboresha ufundishaji wa masomo ya sayansi ambayo hayana walimu wa kutosha katika Tanzania na duniani pote kwa kutumia njia za ufundishaji za kutumia teknolojia ya habari, mawasiliano na teknolojia.

Rais Kikwete pia amekutana na kufanya mazungumzo na Bwana Mark Suzman, Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Taasisi ya Bill and Melinda Gates ya Marekani. Aidha, Rais amekutana na kufanya mazunguzo na Bwana Sunnil Bharti Mittal, Mwenyekiti wa Kampuni ya kimataifa ya simu ya Airtel duniani.