Jumamosi , 16th Apr , 2016

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaambia watendaji na wadau wa mradi Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), kuwa hawana muda wa kulala na kuwataka wakamilishe haraka vipengele vichache vilivyobakia ili mradi huo uweze kuanza kazi haraka iwezekanavyo.

Waziri Mkuu, Majaliwa, na viongozi wenGine wakikagua mabasi yaendayo haraka.

Ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wakuu wa taaasisi, watendaji wakuu na wadau wa mradi huo kwenye kikao alichokiitisha ofisini kwake Magogoni jijini Dar es salaam

Waziri Majaliwa amewataka watu wa DART, UDA-RT eGA, MAXCOM, POLISI NA SUMATRA wafanye kazi kama timu moja na ili maeneo yaliyobakia yaweze kukamilika katika muda mfupi na kuhakikisha wanatoa elimu ya kutosha kwa watumiaji wa barabara hiyo.

Akielezea utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Bw. Ronald Rwakatare amesema miundombinu ya mradi huo imekamilika na utoaji huduma unatarajiwa kuanza hivi karibuni kwani hivi sasa wanamalizia ufungaji wa mfumo wa ukusanyaji nauli na uendeshaji wa mabasi hayo.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa UDA Rapid Transit (UDA-RT), Bw. Robert Kisena amesema mpango wa kuanza kwa mradi huo umekamilika na tayari mabasi yote yamelipiwa kodi pamoja na bima.