Jumatano , 18th Mei , 2016

Serikali imesema kuwa imeshatenga hekari 8,000, nchi nzima kwa ajili ya vijana kufanya shughuli za kilimo na biashara huku serikali ikiendelea kuangalia mashamba mengine kwa ajili ya kuwagawia vijana kwa ajili ya shughuli hizo.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Walemavu Anthony Mavunde.

Akizungumza leo Bungeni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Walemavu Anthony Mavunde, wakati wa kipindi cha maswali na majibu amesema kuwa huo ni kati ya mipango iliyowekwa kwa ajili ya kuwashirikisha vijana katika kukuza uchumi wa nchi kupitia kilimo.

Mhe. Mavunde pia amewataka vijana waliohitimu vyuo vikuu na Elimu ya Juu, kujiunga katika makampuni au vikundi mbalimbali ili waweze kunufaika na mikopo ya serikali inayotolewa ili kuwawezesha vijana kujiajiri na kuacha kusubiri ajira toka serikalini.

Naibu Waziri huyo amesema kuwa serikali inatambua changamoto za wasomi hao hivyo kwa mpango huo na mingine iliyowekwa na serikali itawasaidia kujikwamua kiuchumi na kukuza pato la taifa kwa ujumla.

Mhe. Mavunde amewataka vijana kutumia pia fursa ya mfuko wa maendeleo ya vijana na mikopo inayotolewa na halmashauri kwa kukaa katika vikundi na makampuni mbalimbali yaliyoanzishwa na vijana kwa ajili ya kujikwamua.