Historia inaandikwa - Zitto Kabwe

Tuesday , 13th Jun , 2017

Ikiwa ni siku moja imepita toka Rais John Pombe Magufuli apokee ripoti ya pili ya uchunguzi wa mchanga alimaarufu kama 'Makinikia' Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe amefunguka na kusema historia inaandikwa.

Mbunge wa Singida Mashariki Mhe. Tundu Lissu akiteta jambo na Mbunge wa Kigoma Mjini Mhe. Zitto Kabwe bungeni kipindi cha nyuma.

Zitto Kabwe ameweka picha akiwa bungeni kipindi cha nyuma yeye pamoja na Mbunge Tundu Lissu na kusema siku zote Uzalendo ni kufanya jambo ambalo watu wengi hawakuelewi lakini wewe unajua kuwa ni jambo sahihi na unakubali kutukanwa, kusimangwa, kuzushiwa lakini wewe unaendelea kupambana.

Mbunge huyo anasema hata kama watu watafanya yote hayo na wewe kuendelea kupambana ipo siku watu hao waliokuita msaliti watakuita shujaa huku wale waliokuzomea watakushangilia

"Mwisho wa siku historia inaandikwa tu. Uzalendo ni kufanya jambo ambalo wengi hawakuelewi lakini wewe unajua ni jambo sahihi na unakubali kutukanwa, kususubikwa, kusimangwa, kuzushiwa, lakini Unapambana tu. Mwisho wa siku waliokuita msaliti watakuita shujaa. Waliokuzomea wanashangilia. Wewe unafanya nini? Unakaa kimya kwani kwenye kukaa kimya pia kuna kusema kukubwa zaidi. Muhimu Nchi ifaidike. Huko nyuma nilipata kusema, hata Mungu akinichukua sasa unakwenda ukiwa umetabasamu kwani unakuwa umetimiza wajibu wako duniani" aliandika Zitto Kabwe