Jumamosi , 12th Sep , 2015

RAIS Jakaya Kikwete na Amiri jeshi mkuu leo amewatunuku kamisheni maafisa 166 wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), wa kundi namba 56/14, katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi kilichopo Monduli, Mkoani Arusha.

Amiri Jeshi Mkuu Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiagana na makamanda wakuu wa JWTZ.

Miongoni mwa waliotunikiwa nishani hizo ni wanawake 21 na wanaume 145 ambao kwa pamoja walikula kiapo cha utii na wanafunzi waliofanya vizuri katika mafunzo hayo aliwatunuku zawadi.

Baadhi ya wanafunzi waliofanya vizuri katika mafunzo hayo na kutunukiwa zawadi ni Martina Simba, Nuru Mhama, Sham Mbegu na mshindi wa jumla ni Anthony Shija.

Hii ni Kamisheni ya mwisho kabla ya kuondoka katika kiti hicho, Rais Jakaya Kikwete kuitoa chuoni hapo, ambapo katika uongozi wake aliwatunuku wanafunzi 2,707 ambao ni wanaume na wanawake ni 302 na wanafunzi wanajeshi waliotoka katika nchi mbalimbali walikuwa ni 594 kati yao wanawake ni kutoka nchi mbalimbali za Afrika.

Pia hafla hiyo imehudhuriwa na Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama ,Mawaziri Wakuu wa Vyuo kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pamoja na wananchi mbalimbali.

Rais pia amepewa zawadi mbalimbali kwa kuthamini mchango wake, chuoni hapo yeye pamoja na mkewe, Mama Salma Kikwete.