Jumapili , 7th Sep , 2014

Amiri jeshi mkuu wa Tanzania ambaye pia ni Rais wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete wameyataka majeshi hapa nchini kuendelea kubuni mbinu zaidi zinazokwenda na wakati ili kuweza kukabiliana na vitendo mbalimbali vya kigaidi.

Rais wa Tanzania Dkt Jakaya Kikwete.

Rais Kikwete ameyasema hayo katika kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya jeshi la kujenga taifa iliyofanyika Mkoani Arusha ambapo ameongeza kuwa kwa miaka mingi jeshi hilo limekuwa likifanya vizuri lakini ifike wakati wanajeshi wake wajifunze mbinu za kisasa ili kuweza kukabiliana na matukio yaliyopo kwa sasa.

Kwa Upande wake Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dr. Hussein Mwinyi amesema kwa sasa jeshi hili limepiga hatua kwa kuwa na silaha za kisasa huku changamoto iliyopo ni kuzitunza silaha hizo ambazo zinahitaji gharama.

Wakati huo huo, majambazi wamevamia kituo cha polisi Ushirombo Wilaya ya Bukombe huko mkoani Geita usiku wa kuamkia jana na kuwaua askari polisi wawili na kujeruhi wengine wawili kisha kupora silaha ambazo idadi yake haijafahamika

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Ernest Mangu amesema watu wanaosadikiwa kuwa ni Majambazi walivamia kituo hicho cha polisi usiku na kuanza kurusha risasi pamoja na kulipua bomu la kivita kulikopelekea vifo vya polisi hao na kujeruhi wengine wawili.

IGP Mangu amewataja Polisi waliouawa ni polisi wa kike WP Uria Mwandiga pamoja na PC Dastan Kimati huku waliojeruhiwa ni David Ngupama na Mohammed Hassan na kuongeza kuwa uchunguzi zaidi juu ya tukio hilo unaendelea na kuahidi Zawadi ya sh. Milioni 10 kwa atakaesaidia kufanikisha kukamatwa kwa majambazi hayo.