Ijumaa , 3rd Mei , 2024

Kama ilivyotabiriwa awali, uwepo wa kimbunga “HIDAYA” karibu na pwani ya nchi, umeendelea kutawala mifumo ya hali ya hewa kwa baadhi ya maeneo ambapo katika kipindi cha saa 12 zilizopita, vipindi vya mvua na upepo mkali vimeanza kujitokeza.

Picha za Satelaiti Zikionyesha Mwenendo wa Kimbunga Hidaya

Taarifa ya mwenendo wa kimbunga “HIDAYA” kilichopo katika Bahari ya Hindi mashariki mwa pwani ya nchi kama ambavyoimetolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaeleza kuwa hadi kufikia saa 9 mchana wa leo, Kimbunga hicho kilikuwa katika eneo la bahari takriban kilomita 276 kutoka pwani ya Kilwa (Mkoa wa Lindi) na kilomita 300 kutoka pwani ya Mtwara kikiwa na mgandamizo wa hewa wa kiasi cha 981hPa na kasi ya upepo unaofika kilomita 130 kwa saa.  
 
Katika kituo cha hali ya hewa Mtwara, upepo mkali unaozidi kilomita 40 kwa saa umeweza kupimwa katika nyakati tofauti kuanzia asubuhi ya leo ambapo hali kama hiyo pia imeweza kujitokeza katika vituo vyetu vingine vilivyopo katika ukanda wa pwani kama vile vituo vya hali ya hewa vya Kilwa Masoko, Zanzibar na Pemba. 

Matarajio ni kwamba kimbunga “Hidaya” kitaendelea kusogea kuelekea karibu kabisa na ukanda wa pwani ya nchi yetu usiku wa leo na mchana wa kesho tarehe 04 Mei 2024 kabla ya kuanza kupungua nguvu yake kuelekea siku ya Jumapili tarehe 05 Mei 2024. 

Aidha kwa usiku wa leo na siku ya kesho tarehe 04 Mei 2024, kimbunga “HIDAYA” kinatarajiwa kusababisha matukio ya vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali katika maeneo ya ukanda wa pwani hususan wa mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani na Dar es salaam pamoja na kisiwa cha Unguja. 

Vilevile, matukio ya mawimbi makubwa baharini yanatarajiwa kujitokeza katika ukanda wote wa mwambao wa pwani ya Bahari ya Hindi.