Alhamisi , 29th Jan , 2015

Serikali imewahikikishia watanzania kuwa zoezi la uandikishwaji wa wapiga kura katika daftari la kudumu kwa mfumo wa kieletronik BVR litafanyika kwa ufanisi na ndani ya wakati uliopangwa.

Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda

Akijibu swali la kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni Mh. Freeman Mbowe kuhusu uhakika wa zoezi hilo, Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda amesema tume ya uchaguzi imeihakikishia serikali kuwa vifaa vinavyotarajiwa vina ubora mara ya mbili ya vilivyoletwa kwa ajili ya zoezi ya majaribio.

Licha ya kukiri kuwa awali serikali ilikua na tatizo la kifedha Pinda amesema tume imewahikikishia kuwa zoezi la upigaji kura kwa ajili ya katiba mpya litafanyika katika tarehe iliyopangwa na kwamba uchaguzi mkuu mwezi Oktoba utafanyika bila tatizo lolote.

Akiendelea kumtoa wasiwasi Mh. Mbowe kuhusu ufanisi wa vifaa hivyo vya BVR, Pinda amesema kuwa endapo tume itaona kuwa zoezi hilo haliwezekani kwa sababu yoyote ile, itatoa taarifa serikalini na serikali iko tayari kubadili maamuzi.

Tume ya Uchaguzi ilitangaza kuanza zoezi hilo rasmi kwa awamu ya kwanza Februari 16 hadi Machi 15 mwaka huu na Rais Kikwete alitangaza Kura ya maoni kufanyika April 30 mwaka huu