Alhamisi , 2nd Apr , 2015

Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania (NEC) imesema haitoweza kuendelea na zoezi la kura ya maoni kama ilivyopangwa kufanyika Aprili 30, kutokana na kutokamilika kwa zoezi la uboreshaji daftari la kudumu la wapigakura.

Akiongea leo Jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mstaafu Damian Lubuva amesema kuwa zoezi lolote la kupiga kura likiwepo la kura ya maoni ya Katiba inayopendekezwa, linategemea kuwepo kwanza kwa daftari la kudumu la wapigakura.

Kwa upande wa gharama zilizotumika kununua mashine mpya za BVR Jaji Lubuva amesema kuwa serikali tayari imelipia mashine zote kiasi cha Dola za Kimarekani Milion 72 na tayari zimeshaagizwa kutoka nchini China na muda wowote zitawasili nchini na zitaanza kuendelea na zoezi hilo kwa mikoa ya Ruvuma,Iringa, Mtwara na Lindi.

ZOEZI LA UANDIKISHAJI KUENDELEA HADI JULAI.
Kwa mujibu wa taarifa ya Tume hiyo:-
Zoezi la uandikishaji mkoa wa Njombe litakamilika April 18 na baada ya hapo itafuatia mikoa ya Ruvuma, Iringa, Mtwara na Lindi#ZamuYako2015.
Vifaa vya kuandikishia (BVR kits) nyingine 248 zitawasili ndani ya wiki ijayo na vingine 1600 vitafuata baada ya muda mfupi.
NEC imesema kama vifaa vya kuandikishia vitafika vyote zoezi la uandikishaji litakamilka ifikapo mwezi julai mwaka huu.
Gharama za vifaa vyote vilivyoagizwa kwaajili ya vifaa vya kuandikishia (BVR kits) ni dola za Kimarekani milioni 72 ambazo ni sawa na Tsh bilioni 133.4