Jumanne , 20th Jan , 2015

Kamati ya bunge ya hesabu za serikali za mitaa LAAC imeazimia kupeleka hoja mahususi bungeni ili ijadiliwe na Bunge zima juu ya matumizi mabaya ya fedha za wananchi katika halmashauri nyingi nchini Tanzania.

Akitangaza maazimio hayo leo mwenyekiti wa kamati hiyo Rajabu Mbarouk amesema wamechoshwa na wizi pamoja na matumizi mabaya ya fedha za watanzania yanayofanywa na watendaji wa halmashauri.

Mbali na wizi na matumizi mabaya, Mbarouk amesema kuwa wamechoshwa pia na tabia halmashauri hizo kutopeleka fedha za vijana na wanawake kwa ajili ya kuwawezesha huku fedha nyingi zikitumika bila kuwepo na risiti na miradi mingi kutekelezwa chini ya viwango.

Mh Mbarouk ameongeza kuwa suala hilo litakuwa ni hoja ya bunge zima na serikali lazima waje na majibu juu ya jambo hili sugu nchini.

Wakati huo huo.......
Waziri wa Fedha na Uchumi nchini Tanzania Mh. Saada Mkuya Salum amezitaka Halmashauri zote nchini kukusanya mapato ambayo sio ya kikodi na kuendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato na sio kutegemea Fedha toka serikali kuu.

Akijibu swali kuhusu Halmashauri kukosa fedha za miradi ya maendeleo wakati akiongea na Hotmix Waziri Mkuya amesema kuwa ni kweli bado hali ya kifedha sio nzuri sana nchini kwani bado Wafadhili hawajatimiza ahadi zao huku Halmashauri nyingi zikishindwa kukusanya mapato ya kutosha ikiwemo mapato yasio ya kodi.

Akizungumzia suala la kuendelea kuwepo kwa mishahara hewa serikalini Waziri Mkuya amesema bado kuna changamoto ya baadhi ya maafisa wa mabenki ambao sio waaminifu wanaoshirikiana na maafisa wa serikalini kuendelea kupokea mishahara hewa kwa njia mbalimbali kama vile kuendelea kuwalipa watumishi ambao wameshastaafu na hata waliokufa na wengine kuwa na akaunti mbilimbili