Ijumaa , 13th Nov , 2015

Wilaya ya Bahi mkoa wa Dodoma, imepiga marufuku upikwaji wa pombe za kienyeji kufuatia wilaya hiyo kukumbwa na ugonjwa kipindupindu.

Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Francis Mwonga, akiongea na wananchi wa Kijiji cha Mtitaa

Akizungumza na East Afrika Radio Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Fransis Mwonga amesema kuwa wameamua kuchukua hatua hiyo ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukabiliana na ugonjwa huo ambao umegharimu baadhi ya maisha ya watu.

Mwonga amesema kuwa hatua hizo zitasaidia kwa namna moja ama nyingine kupunguza kasi ya uenezwaji wa ugonjwa huo.

Mwonga ametoa wito kwa jamii kuendelea kuzingatia suala la usafi ambalo ni jambo muhimu katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa kaimu mganga mkuu wa wilaya hiyo Dkt. Gerald Maro ni kwamba mpaka sasa wagonjwa walioongezeka ni 9 na kati ya hao waliolazwa katika kambi maalum ya wagonjwa hao iliyopo Mpamantwa ni 2 ambapo awali walikuwa na wagonjwa 87 lakini kwa sasa wapo 96.

Dkt. Maro amehimiza matumizi ya vyoo bora, kuzingatia kanuni za usafi wa mazingira na matumizi ya maji safi na salama ya kunywa.

Kwa upande wake mganga mkuu wa wilaya ya Dodoma mjini Dkt. James Charles ameeleza hali ilivyo kwa sasa na kusema katika kambi maalum waliyoiweka eneo la Nanenane idadi ya wagonjwa imepungua kutoka saba waliokuwa awali na kubaki 6.

Ugonjwa huo uliripotiwa kuingia katika wilaya ya Kongwa, Chemba, Bahi, Chamwino na Manispaa ya Dodoma na kusababisha watu wanne kupoteza maisha.