Ijumaa , 5th Aug , 2022

Meli tatu zilizobeba shehena za nafaka kwa ajili ya soko la kimataifa zimeondoka leo nchini Ukraine.

Meli hizo zilizobeba zaidi ya tani 57,000 za nafaka za Ukraine ziliondoka katika bandari za Bahari Nyeusi chini ya makubaliano ya karibuni kati ya Moscow na Kyiv yanayolenga kutuliza mzozo wa uhaba wa chakula duniani.

Serikali ya Kyiv imesema meli mbili zilizobeba mahindi ya Ukraine moja inayopeperusha bendera ya Malta na nyingine ya Kituruki -- ziliondoka bandari ya Chornomorsk wakati nyingine inayopeperusha bendera ya Panama iking'oa nanga katika bandari ya Odessa.

Lakini hatua hiyo imegubikiwa na ripoti ya Shirika la Amnesty International iliyoorodhesha matukio katika miji 19 ambako wanajeshi wa Ukraine walidaiwa kuwaweka raia katika mazingira ya hatari kwa kuweka ngome zao katika maeneo ya makaazi.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amepinga tuhuma hizo akisema shirika hilo linataka kulisamehe taifa la kigaidi na kuelekeza lawama kutoka kwa mchokozi hadi kwa mwathiriwa.