Jumatano , 15th Jul , 2015

Jeshi la polisi mkoani Mwanza, linamshikilia mmiliki na mkurugenzi wa kampuni ya mabasi ya J4 Express yanayofanya safari zake Mwanza- Kampala na Mwanza- Musoma, Juma Mahende, mkazi wa Nyakato jijini hapa kwa tuhuma za kuwaua kwa bastola wakazi wawili

Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza, CP Charles Mkumbo.

Mauaji hayo yalifanywa kwa marehemu Ally Abeid mkazi wa Igoma na Claude Sikalwanda wa Nyasaka katika tukio lililotokea saa 4 usiku Nyakato sokoni jijini Mwanza.

Akizungumza na Earadio leo huku akibubujikwa na machozi, kaka wa marehemu Abeid, Ramadhani Abeid, alisema tukio hilo limetokea katika mazingira ya kutatanisha kutokana mmiliki huyo kufahamiana na marehemu hao.

“Mdogo wangu (Abeid), alikuwa anamdai mtuhumiwa huyo lakini tunashangazwa na huyu J4 kuamua kuchukua maamuzi haya ya mauaji kuua ndugu yetu…tunaomba polisi wasipindishe tukio hili,” alisema Abeid.

Alisema mtuhumiwa huyo alifanya tukio hilo wakati marehemu wote wakiwa hawana silaha zozote mikononi mwao.

Naye dada wa marehemu Sikalandwa, Aziza Steven, alisema kifo cha kaka yake kimeacha pengo kubwa katika familia yao kutokana na kuwa tegemeo la familia.

Akizungumza huku akibubujikwa na machozi, Aziza alisema tukio lililofanywa na mmiliki huyo wa mabasi, unyama mkubwa kwani marehemu hao inasemekana walikuwa wanamdai J4, badala ya kupewa chao wanaishia kuuawa.

“Tunaomba vyombo vya dola kuhakikisha vinatenda haki katika uchunguzi wa suala hilo, kwani hawa ndugu zetu kabla ya kwenda kwa mtuhumiwa huyo waliaga wakidai wamepigiwa simu ili kulipwa madai yao,” alisema Aziza.

Dominata Gabriel ambaye ni mjane wa mjane wa marehemu, Ally Abeid, alisema haamini kama mumewe ameuawa na mtuhumiwa huyo kutokana na wawili hao kufahamiana kwa muda mrefu.

“Siamini kama mzazi mwenzangu amefariki kwani walikuwa wanafahamiana kwa muda mrefu…sielewi kabisa kilichotokea mpaka sasa,” alisema mjane huyo, Dominata.

Mmiliki wa nyumba aliyokuwa akiishi marehemu Abeid huko Igoma, Roger Rwegasira, alisema alipokea taarifa hizo za kuuawa kwa mpangaji wake kwa kushitukiza.

“Usiku wa juzi tulionana, lakini sikufahamu tena kinachoendelea hapo hadi nilipopata taarifa alfajiri ya kuuawa kwake…inatia simanzi sana kuhusiana na mauaji haya,” alisema Rwegasira.

Hata hivyo, kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo, alithibitisha kutokea tukio hilo na kuelezea mazingira ya vifo vya watu hao ambao waliuawa kwa kupigwa risasi kifuani.

Kamanda Mkumbo alisema tukio hilo lilitokea mtaa wa Nyakato Sokoni baada ya Luhende kuwapiga risasi marehemu hao kifuani na kufariki papo hapo.

“Saa 4 usiku Julai 13 mwaka huu, mkurugenzi wa kampuni ya mabasi J4 Express akiwa anajiandaa kufunga ofisi yake, alikutana na watu wawili Ally Mohamed (35) na Claude Steven (35), ghafla ukaanza mzozo uliopelekea Luhende kuwapiga risasi na kufariki papo hapo,” alisema Mkumbo.

Aidha, kamanda Mkumbo alisema mtuhumiwa huyo alifanya mauaji hayo kwa kutumia bastola aina ya Brown namba 00092890, huku polisi ikisema inaendelea na uchunguzi wa chanzo cha mauaji hayo.