Jumatano , 28th Jan , 2015

Mgomo wa wafanyabiashara ulioanzia jijini Dar es Salaam umeathiri na mikoa mingine huku viongozi wa jumuia ya wafanyabiashara nchini wakidai kuwa hawajui ni lini watafungua maduka yao hadi watakapoelezwa kiini cha mwenyekiti wao kukamatwa.

Hali ilivyo katika maeneo ya Kariakoo

Mgomo wa wafanyabiashara ulioanzia jijini Dar es Salaam umeathiri na mikoa mingine huku viongozi wa jumuia ya wafanyabiashara nchini wakidai kuwa hawajui ni lini watafungua maduka yao hadi watakapoelezwa kiini cha mwenyekiti wao kukamatwa.

Katika jiji la Dar es Salaam EATV imeshuhudia maduka yakiwa yamefungwa ambapo wananchi waliokuwa wanafika maeneo hayo pamoja na vijana walioajiriwa kwenye maduka hayo hasa Kariakoo wamelalamikia kitendo hicho na kudai kuwa kinawaathiri kwa kiasi kikubwa kwani wana familia zinawategemea.
 
Kwa upande wao wafanyabishara ndogondogo maarufu wamachinga nao wamelalamikia kitendo hicho kwa madai kuwa wanategemea maduka hayo kununua bidhaa ili wakatembeze mitaani hivyo hali hiyo inawarudisha nyuma kimaendeleo.
 
Msemaji wa jumuia hiyo Bw Stephen Chamle amekiri kuwa hali hiyo pia inawaathiri kwani wana mikopo wanatakiwa kurejesha lakini wamelazimika kufanya hivyo kutokana na mfumo wa ulipaji kodi uliopo hivi sasa ambao siyo rafiki kwa wafanyabiashara.

Baadhi ya mikoa ambapo migomo hiyo imetokea ni pamoja na Dodoma, Ruvuma na Mbeya.