Jumatatu , 13th Apr , 2015

Miili ya watu 15 kati ya 19 waliopoteza maisha katika ajali ya basi na lori mkoani Morogoro imezikwa leo katika makaburi ya Pamoja ya Msanvu wilayani Kilosa mkoani humo.

Mamia ya wakazi wa wilaya za Kilosa na Kilombero wamejitokeza katika mazishi ya pamoja ya watu 15 kati ya 19 waliofariki katika ajali ya basi ya Nganga ambalo liligongana na fuso kisha kuwaka moto katika eneo la Iyovi na kuzikwa katika kaburi la pamoja kwenye makaburi ya Msamvu Ruaha wilayani Kilosa mkoani Morogoro.

Wakizungumza kwa niaba ya serikali ya mkuu wa wilaya ya Kilosa John Henjewele amesema serikali imewalazimu kufanya mazishi ya pamoja ya watu waliofariki kwenye ajali hiyo ambao miili yao haijatambulika.

Pia amesema serikali itaendelea na zoezi la ukaguzi wa magari mkoani wa Morogoro ili kudhibiti ajali za mara kwa mara na kupoteza maisha ya watu huku wengine wakiachwa na vilema vya maisha.

Naye mkuu wa wilaya ya Kilombero Lephy Gembe amewataka wananchi kuwa na uvumilivu katika msiba mkubwa walioupata.

Kwa upande wake diwani wa kata ya Ruaha Rahel Nyangasa amesema wamepokea msiba huo kwa masikitiko makubwa kwani umekuwa ni pigo kubwa kwa wakazi wa wilaya hizo.

Ndugu na waombolezaji nao wamesema msiba huo si wakusahaulika kwani umewashtua sana na muinjilisti wa kanisa la kiinjili la kilutheri Issaya Chura akiomba serikali kuendelea kukabiliana na madereva wabovu.