Jumanne , 10th Feb , 2015

Jengo la ghorofa tatu la Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lililopo Mtaa wa Mosque na Libya eneo la Kitumbini katikati ya Jiji la
Dar es Salaam limeungua moto leo na kusababisha hasara ya mali ambayo thamani yake haijajulikana mara moja.

Askari wa Jeshi la Zima moto akiwa kazini

Vikosi vya zimamoto vilivyofika katika eneo hilo vilionekana kushindwa kuuzima moto huo ulioanza majira ya saa sita mchana, katika ghorofa ya tatu ya jengo hilo ambalo sehemu ya juu inatumika kwa makazi ya watu na ofisi.

Magari mawili ya kwanza ya zimamoto yaliyofika katika eneo la moto, yalishindwa kuudhibiti moto huo kutokana na kuwa na maji kidogo na mipira kupasuka ambapo maji hayo yalitumika kwa muda kidogo na kuisha kabla ya kuuzima moto huo, hali iliyoibua hasira za wananchi waliokuwepo kushuhudia tukio hilo.

Akizungumza leo na waandishi wa habari katika eneo la tukio Kamanda wa Kanda Polisi Maalum ya Dar es Salaam, Kamishina Suleiman Kova amesema vikosi vya uokoaji na Zimamoto vimefanya ushirikiano katika kuzima moto huo baadhi ya maeneo na kuokoa maduka katika majengo hayo.

Kova amesema kuwa vikosi vya ukoaji vya zima moto vimefanya kazi kwa ushirikiano ambavyo ni Zimamoto za Uwanja wa Ndege, Zimamoto ya Kampuni ya Ulinzi ya Ultimate, Night Support, pamoja na Kikosi cha Zimamoto ya Jiji. Amesema kuwa chanzo cha moto bado hakijafahamika mpaka sasa na uchunguzi wa kubaini chanzo cha moto huo bado unaendelea.

Naye Kamishna msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji Kanda Maalum ya Dar es salaam, Jeswald Nkongo amewataka wananchi kutoa taarifa mapema pindi waonapo matukio ya moto na sio kudharau kwa kuamini kuwa moto ni mdogo na wanaweza kuudhibiti.