Jumamosi , 21st Nov , 2020

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi, amewaagiza mawaziri wake kuhakikisha wanafuatilia kwa ukaribu miradi yote yenye udanganyifu, ukiwemo ule wa kutotoresha vifaranga vya samaki uliokutwa na samaki watano pekee.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi.

Kauli hiyo ameitoa hii leo Novemba 21, 2020, Ikulu ya Zanzibar, wakati akizungumza na mawaziri aliowaapisha ambapo amewapa maelekezo mbalimbali ya kuzingatia na kufuata ikiwemo kukomesha masuala ya rushwa, kuzingatia usafi maofisini mwao pamoja na kuzijua wizara wanazofanyia kazi.

"Kwa siku chache nilizokaa ofisini nimetembelea baadhi ya maeneo na nimesikitishwa na kiwango cha miradi, nimekwenda hospitali ya Mnazi Mmoja kuna mradi wa jengo la macho, mpaka leo haifanyi kazi sababu kuna beseni moja la madaktari kujiosha kabla ya kuingia chumba cha kufanyiwa operesheni halijawekwa na mkandarasi ameshalipwa pesa zote", amesema Dkt. Mwinyi.

"Makamu wa Pili wa Rais amekwenda kuangalia mradi wa kutotoresha vifaranga vya Samaki, tukiwa field tunazungumza na watu tunawaambia kwamba tutazalisha vifaranga Milioni 1, alichokiona jana pale samaki watano, majongoo watatu, kaa mmoja haiwezekani nahitaji ripoti ya kina juu ya mradi ule, fedha zilizotumika na kwanini uko namna ile mara moja", ameongeza Dkt. Mwinyi.