Jumamosi , 27th Aug , 2016

Rais Yoweri Museveni wa Uganda amesema bara la Afrika linakabiliwa na changamoto 11 (strategic bottlenecks) ambazo zinakwamisha maendeleo ya bara hilo na akataka zitafutiwe ufumbuzi ili kuzisaidia nchi nyingi barani humo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni kabla ya kuanza kwa Mkutano wa African Peer Review Mechanism Forum (APRM)kwenye ukumbi wa hoteli ya Intercontinental jijini Nairobi Agosti 26, 2016.

Rais Museveni amezitaja changamoto hizo wakati akiwasilisha mada binafsi katika Mkutano wa 25 wa Wakuu wa Nchi wanachama wa Mpango wa Kujitathmni Kiutawala Bora barani Afrika (APRM Forum) uliofanyika kwenye hoteli ya InterContinental jijini Nairobi, Kenya.

Rais Museveni amesema kwa zaidi ya miaka 50, amekuwa kiongozi katika sehemu kadhaa na kwamba amebaini kuwa changamoto hizo zimezuia ukuaji wa uchumi barani Afrika pamoja na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii.

Alisema asilimia kubwa ya changamoto hizo haikupata ufumbuzi hata wakati malengo ya maendeleo ya milenia (MDGs) yalipokuwa yanatekelezwa.

Alizitaja changamoto hizo kuwa ni mikanganyiko ya kiitikadi ambayo huzaa ubinafsi na maslahi binafsi; kuwepo kwa mataifa dhaifu (weak states); nguvukazi duni (kitaaluma na kiafya), uduni wa miundombinu (barabara, maji, umeme, tehama) ambao unashindwa kuvutia uwekezaji; uhaba wa viwanda unaolazimisha nchi kusafirisha mali ghafi na uhaba wa masoko ya bidhaa zinazozalishwa barani Afrika.

Changamoto nyingine ni uduni wa huduma za kijamii unaosababisha huduma mbovu kwenye maeneo ya utalii, mabenki na mahoteli; kilimo duni kisichotumia mbolea, dawa za kuua wadudu, mbegu za kisasa au njia za umwagiliaji; makosa ya kisera kama vile ubinafishaji au utaifishaji mali zinazomilikiwa na sekta binafsi; ukandamijazi wa demokrasia na ukosefu wa maadili miongoni mwa watumishi wa umma.

Naye Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini alisema kwa vile changamoto hizo zinagusa nchi nyingi za Afrika, ni vema iundwe timu ya wataalamu watakazipitia zote na kuainisha zipi zinafaa kufanyiwa kazi na kisha taarifa yao iwasilishwe kwenye kikao kijacho cha Wakuu wa Nchi wanachama.

Akifunga mkutano huo, Rais Kenyatta aliitaka sekretarieti ya APRM ipitie changaoto hizo na kuziwakilisha kwenye kikao chao kijacho ambacho alisema kitafanyika Januari 2017, mjini Addis Ababa, Ethiopia katika tarehe itakayopangwa baadaye.