Jumanne , 23rd Jun , 2015

Mwanamke mwingine amejitokeza kuchukua fomu ya kuwania urais kupitia CCM ambapo amekuwa ni mwanamke wa tano kuchukua fomu katika kuwania kinyang’anyiro hicho.

Ritha Ngowi ambaye ni Ofisa Maendeleo ya jamii

Mwanamke huyo ni Ritha Ngowi ambaye ni Afisa Maendeleo ya jamii amesema kuwa anaweza kuwatumikia na kuwaongoza wananchi wa Tanzania kwani amekuwa katika eneo la kufanyakazi na jamii kwa muda mrefu.

Ameeleza vipaumbele vyake Ngowi amesema kuwa akifanikiwa kupita katika kinyang’anyiro hicho atahakikisha ataboresha sekta ya elimu na uchumi.

Amesema kuwa atahakikisha kuwa anaboresha sekta ya elimu ili iweze kumfikia kila mtanzania kupata elimu angalau ya msingi na kuachana na habari ya watu kukaa bila chochote cha kufanya.

Aidha katika sekta ya uchumi amesema kuwa ataimarisha kilimo kwa kutoa elimu bora ya kilimo na zana bora kama pembejeo ili kukuza kilimo na kukuza uchumi wa nchi.

Wakati huo huo wawania urais watatu kupitia CCM wamerudisha fomu zao leo baada ya kukamilisha zoezi la kuwapata wadhamini katika mikoa 15 ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Waliorejesha fomu zao leo ni pamoja na Balozi Ally Karume, Dk. John Magufuli na Steven Wassira.