Jumatano , 31st Jul , 2019

Mkuu wa Wilaya ya Hanang Joseph Mkirikiti, ameikaribisha vizuri timu ya Namthamini kutoka East Africa Television na East Africa Radio, ambapo amekubali kuongozana na timu kwenda shule ya Sekondari Simbai.

Akiongea ofisini kwake amesema amefurahi kuona Wilaya yake imekuwa ya kwanza kufikiwa na mgawo wa taulo za kike kupitia Kampeni ya Namthamini kwa mwaka 2019.

''Karibuni sana sisi tumefurahi mmetuchagua kuwa wa kwanza, ikiwesekana sasa tuwe wadau wenu wa kudumu''. Amesema Mkirikiti.

Aidha mkuu huyo wa Wilaya amekubali kwenda shuleni kuongoza zoezi la kugawa taulo hizo katika shule ya Sekondari Simbai akiongozana na Kamati ya Usalama ya Wilaya ambayo leo ilikuwa na kikao ofisini kwake ikiongozwa na yeye ambaye ni Mwenyekiti.

Awali Afisa Elimu wa Hanang Mwalimu Elizabeth Lussingu pamoja Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Pantaleo Mkangala walieleza furaha yao juu ya ujio wa taulo hizo za kike.

''Huu ni msaada mkubwa sana kwetu kama Halmashauri na itasaidia sana kupunguza tatizo wa wasichana kukosa masomo wawapo kwenye hedhi'', alisema Lussingu.