Ijumaa , 18th Sep , 2015

Viongozi wa juu wa Chama cha NCCR-Mageuzi, akiwemo Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu na Wajumbe wa Halmashauri kuu ya Chama hicho wameelezea kutoridhishwa na ushirikiano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Katibu Mkuu wa NCCR-MAGEUZI, Mosena Nyambabe akizungumza na waandishi wa habari

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam katibu Mkuu wa chama hicho Mosena Nyambabe amesema chama hicho kinapewa ushiriki mdogo ndani ya Umoja huo lakini pia kukiukwa kwa makubaliano waliyowekeana tangu awali.

Nyambane amesema katika makubaliano ya awali walipewa majimbo 12 kusimamisha wagombea lakini kati ya hao kuna majimbo sita ambayo Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA nao wamesimamisha hali inayowafanya kuona kuna viashiria vya kugeukwa pindi watakapotwaa madaraka

Naye Makamu mwenyekiti wa chama hicho bara Bi. Leticia Ghati Mossore ameongeza kuwa licha ya kusimamisha wagombea hao sita katika majimbo hayo bado katika majimbo mengine sita yaliyobaki wanafanyiwa fujo na chama hicho ikiwemo kuwakataa mbele ya mikutano.

Aidha makamu huyo mwenyekiti amemtaka mwenyekiti wa chama hicho ndugu James Mbatia aweze kuitisha mkutano wakKikatiba ili kuweza kujadili hatma ya chama hicho baada ya uchaguzi mkuu.

Aidha viongozi hao wamemuonya mwenyekiti huyo kuacha kuwa msemaji wa mambo ya CHADEMA au UKAWA huku akiacha maslahi ndani ya chama chake yakipotea kwa kufuata mkumbo ambao unaweza kukipoteza kabisa chama hicho.

Hata hivyo Mwenyeki wa chama hicho ndug James Mbatia anatarajia kuongea na waandishi wa habair ili kutolea ufafanuzi juu ya suala hilo.