Ndugai aeleza kinachoendelea sakata la wabunge 19

Jumatatu , 30th Nov , 2020

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, amesema kuwa wabunge wote ambao tayari wamekwishaapishwa, wanatambulika kwamba ni wabunge kamili wakiwemo hata wale wabunge wa viti maalum kutoka CHADEMA ambao wamefukuzwa uanachama na chama chao.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai.

Kauli hiyo ameitoa hii leo Novemba 30, 2020, mara baada ya kuwaapisha wabunge wawili walioteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli, ambao ni Hamphrey Polepole na Riziki Lulida.

"Wabunge wote wa Bunge la 12 tuliowaapisha tunaendelea kuwatambua kwamba ni wabunge kamili wote ikiwa ni pamoja na wale 20 wa chadema, 19 wa viti maalum na yule mmoja aliyechaguliwa, Mh. Aida Khenani, nashangaa wanawasonga tu hawa 19 yule mmoja wamemgwaya wakiweza wamfukuze basi", amesema Spika Ndugai.

Aidha Spika Ndugai amempa onyo Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe, kuacha tabia yake ya kuwadhalilisha wanawake hadharani, "Hamjui kwanini wale 19 wamepitia mapito gani, hamjui kwanini imekuwa hivyo, yako mambo hatuwezi kusema humu, viko vyama ni kampuni ya mtu, mtu ni Mungu mtu  bila yeye hakiwezekani chochote, namuambia hawa 19 ni wabunge labda wao kwa kutumia utaratibu wa kikatiba wajiuzulu, lakini kwa yeye na Mnyika wake wale ni wabunge".