"Nilitaka nitoe demo kwa RC hadi Mwenyekiti"- JPM

Jumatano , 24th Feb , 2021

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli, amempongeza mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Aboubakar Kunenge, kwa hatua za haraka alizozichukua za kuanza kujenga shule ya msingi King'ongo ambayo majengo yake yalikuwa yamechakaa na wanafunzi kukaa chini.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli

Kauli hiyo ameitoa hii leo Februari 24, 2021, jijini Dar es Salaam, wakati akizindua barabara za juu za Ubungo, ambazo ameelekeza ziitwe barabara za juu za Kijazi, ikiwa ni hatua ya kumuenzi aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, aliyefariki dunia hivi karibuni.

"Ninashukuru RC ulivyohamia kwenye ile shule lakini kwakweli ile shule ingekuwa mpaka leo haijajengwa nilitaka nitoe demo ningeanzia mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya, mkurugenzi, mpaka mwenyekiti wa kijiji sababu wananchi hawa waliotuchagua wanataka waone matokeo ya yale tuliyoyaahidi", amesema Rais Magufuli

Aidha Rais Dkt. Magufuli, ameongeza kuwa "Kwahiyo mkuu wa mkoa nakushukuru malaika walikugusa ukawahi haraka haraka, nikawa nakuangalia nikasema Kunenge oyee!, kwa sababu mkuu wako wa wilaya alikuwa kashaanza kulalamika kwamba hawa wanatumiwa"