Jumatatu , 14th Sep , 2020

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, leo Septemba 14, 2020, imeahirisha kesi inayowakabili Tundu Lissu na wenzake ya kuandika habari za uchochezi kinyume na sheria ya magazeti ya mwaka 2002, baada ya washitakiwa wawili kushindwa kufika mahakamani.

Tundu Lissu.

Washtakiwa ambao hawakufika mahakamani hapo ni pamoja na mgombea Urais kupitia CHADEMA Tundu Lissu na Ismail Mehboob.

Akizungumza mahakamani hapo mdhamini wa Tundu Lissu ,Robert Katula amedai kuwa amejitahidi kumtafuta mshitakiwa huyo lakini hakumpata.

"Nimejaribu kuwasiliana nae sijampata mpaka sasa hivi, nimeongea na rafiki zake wamesema amebanwa na ratiba ya Tume ya Uchaguzi hivyo tunaomba Mahakama ipange tarehe nyingine", amesema Katula

Kwa upande wake Wakili Mwandamizi wa Serikali, Wankyo Simon wakati akizungumza mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo Thomas Simba, amesema kuwa shauri hilo lilifikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa na kuomba ipangwe tarehe nyingine.

Ambapo Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 15, 2020, itakapotajwa tena ambapo washtakiwa wote wapo nje kwa dhamana.

Katika kesi ya msingi Lissu na wenzake wanakabiliwa na mashtaka matano likiwemo la kupanga njama za kuchapisha taarifa za uchochezi.