Jumanne , 18th Oct , 2016

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imemchagua Mhe. Naghenjwa Kaboyoka Mbunge wa Same Mashariki (Chadema) kuwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo.

Kamati ya PAC, katika kikao chake chini ya mwenyekiti mpya

Tangu kuundwa kwa Kamati hiyo ambayo kwa mujibu wa Kanuni za Bunge inatakiwa kuongozwa na Upinzani ilikuwa bado haijamchagua Mwenyekiti na hivyo ilikuwa chini ya Uongozi wa Makamu Mwenyekiti Mhe. Aeshi Hilaly (Mb).

Katika uchaguzi huo Mhe. Kaboyoka hakupigiwa kura badala yake alipendekezwa na Wajumbe wa Kamati hiyo ambapo wote waliridhia awe Mwenyekiti wao.

Kamati hiyo ilikutana katika kikao chake cha kwanza chini ya Mwenyekiti Mhe. Kaboyoka ambapo mara baada ya kufanya uchaguzi huo ilijadili Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu Hoja za Ukaguzi kwa Mashirika yaliyoko chini ya SUMA JKT.

Wajumbe wa Kamati hiyo walisema hesabu za mashirika hayo hazijazingatia sheria na utayarishaji wa hesabu na kwamba matumizi yao yamezidi bajeti iliyoidhinishwa.

Kamati hiyo ilitoa ushauri kwa SUMA JKT kuhakikisha wanaajiri wahasibu wenye ujuzi badala ya kuajiri watu ambao hawana ujuzi wa kuandaa taarifa za fedha.

Kwa upande wake Mkuu wa Kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Brigedia Jenerali Michael Isamuhyo alikiri kuwepo kwa mapungufu hayo na kwamba kwa sasa Jeshi hilo limepeleka maombi Wizarani kuomba kutenganisha shughuli za SUMA na JKT.

Wakati huohuo , Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) jana ilipokea majumuisho ya shughuli za Kamati kwa kipindi cha kuanzia Agosti 15, 2016 hadi Septemba 2, 2016.

Aidha, Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa jana ilipokea maelezo kuhusu shughuli za Kamati katika kipindi cha Oktoba 17 haadi 30, 2016.

Mhe. Naghenjwa Kaboyoka, Mwenyekiti mpya wa PAC