Jumatatu , 5th Jan , 2015

Jeshi la Polisi kanda maalum ya Dar es salaam linawashikilia vijana 510 wa kikundi cha uhalifu linachojiita panya Road wakiwemo viongozi watatu wa kikundi hicho.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam Kamishna Suleimani Kova akionesha picha za watuhumiwa mbele ya waandishi wa habari

Hatua imekuja kutokana na Oparesheni iliyofanywa na jeshi hilo kufuatia uhalifu, hofu na taharuki waliyosababisha siku ya Ijumaa katika maeneo mbalimbali jijini Dar es salaam.

Akizungumzia Oparesheni hiyo iliyofanyika jijini Dar es salaam ya kuwakamata vijana hao, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam Kamishna Suleimani Kova amesema msako huo umefanyika katika maeneo mbalimbali ya jiji ikiwa ni pamoja na msako wa nyumba kwa nyumba, katika vijiwe vyao na katika vituo vya dalaladala ambako walikamatwa wakiwa wanapiga debe.

Kamishna Kova amesema baadhi ya vijana hao wamekamatwa wakiwa na vichocheo vya uhalifu ambavyo ni pamoja na misokoto ya bangi na Pombe haramu ya Gongo na wakati wowote watafikishwa mahakamani na kufunguliwa mashtaka ya kufanya uhalifu.

Amesema vichocheo vya uhalifu walivyokamatwa navyo ni pamoja na
Puli za bangi 113
Kete za bangi 676
Misokoto ya bangi 294.
Mirungi bunda 03 na
Gongo lita 150

Kamishna Kova amewataja viongozi hao watatu wa Panya Road kuwa ni Halfan Nurdin miaka 24 mkazi wa tandale Sokoni, Said Mohamed miaka 22 mkazi wa Tandale Sokoni na Mohamed Nangula miaka 19 mkazi wa Mburahati kwa Jongo.