Jumamosi , 19th Sep , 2015

Waziri Mkuu Mizengo Pinda amepokea misaada ya zaidi ya sh. milioni 330 kwa ajili ya shule ya msingi Kakuni, iliyopo kijiji cha Kibaoni, wilayani Mlele, mkoa wa Katavi.

Waziri Mkuu, Mhe Mizengo Pinda (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watendaji wa Benki ya NMB mara baada ya kupokea vifaa mbalimbali

HUAWEI na NMB zimetoa msaada huo ikiwa ni sehemu ya mchango wao katika shule mpya ya msingi Kakuni ambayo Waziri Mkuu Mizengo Pinda alianzisha wazo la kuijenga kama njia ya kumshukuru Mungu na kuwashukuru wananchi waliosaidia kumfikisha hapo alipo. Waziri Mkuu Pinda alisoma darasa la kwanza hadi la nne katika shule ya msingi Kakuni mwaka 1957 hadi 1960.

Akizungumza kwenye hafla fupi ya makabidhiano ya msaada huo yaliyofanyika leo mchana (Ijumaa, Septemba 18, 2015) kwenye ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Meneja Uhusiano wa kampuni ya HUAWEI, Bw. Jin Liguo alisema kampuni yake inaamini msaada huo utasaidia kupunguza tofauti za kiteknolojia zilizopo kwenye sekta ya elimu.

“Kampuni ya HUAWEI iko Tanzania tangu 2001 na imedhamiria kufanya kazi na wanajamii kila inapoona imepata fursa ya kufanya hivyo, na hasa katika elimu ambako pia tumelenga kupunguza tofauti za kiteknolojia zinazojitokeza kwenye sekta hiyo,” alisema Bw. Liguo.

Kampuni hiyo imetoa kompyuta za mezani 50, HUAWEI Tablets 100, Laptop tano, Printers mbili, Scanner mbili, Projector mbili, Projector Screens mbili, Power System seti moja na Audio System seti moja vyote vikiwa na thamani ya Dola za Marekani 150,000 (sawa na sh. milioni 300).

Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya NMB, Bw. Waziri Barnabas alisema benki hiyo imelenga kukuza michezo shuleni na ndiyo maana imeamua kutoa msaada wa vifaa vya michezo kwa shule hiyo ya Kakuni.

Benki ya NMB imetoa kompyuta nne; jezi za michezo jozi 192 (soka 72, wavu 40, kikapu 40 na pete 40); mipira 40 (soka 10, wavu 10, kikapu 10 na pete 10). Pia imepanga kuchangia ununuzi wa madawati yenye thamani ya sh. milioni 10 ambayo alisema yapo tayari ila yanasubiri ujenzi wa kituo cha walimu ukamilike. Vifaa hivyo vina thamani ya sh. Milioni 30.

Akizungumza katika hafla hiyo fupi, Waziri Mkuu Pinda aliwashukuru wawaklishi wa HUAWEI na Benki ya NMB kwa msaada huo ambao alisema utachangia kwa kiasi kikubwa kuitimiza ndoto yake aliyokuwa nayo ya kuisaidia jamii iliyomsomesha.

“Wazo la ujenzi wa shule mpya ya msingi Kibaoni lilitokana na ukweli kwamba nilisoma na kumaliza kwenye shule hii ya Kakuni. Nikiwa ni mtumishi wa Serikali, ni Mbunge na sasa hivi ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nilijiuliza hivi shule hii ninaweza kuiacha hivi hivi? Hakuna jambo ambalo naweza kufanya na kuisaidia jamii ya wanakijiji na kata nzima ya kwetu?,” alisema Waziri Mkuu katika mada fupi aliyoiwasilisha leo mbele ya waandishi wa habari.

“Niliwaza pia kufanya ukarabati lakini nikabaini kuwa eneo la shule halitoshi kwani wanafunzi waliopo ni wengi kuliko eneo la shule hiyo. Hivi sasa shule ina wanafunzi wapatao 800. Madarasa yamechakaa na nyumba za walimu pia zimechakaa,” aliongeza.

Waziri mkuu alisema alipeleka maombi kwenye serikali ya kijiji cha Kibaoni ambayo ilitoa ekari 65 kutoka eneo lililokuwa ni mashamba ya bega kwa bega na kisha akawasilisha ombi maalum kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda (wakati huo) ambayo hivi sasa ni Mlele ili kuomba ushauri na usimamizi wa jumla katika kuisimamia ndoto aliyokuwa nayo.

Alisema aliishirikisha halmashauri kuandaa michoro inayotolewa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na OWM-TAMISEMI, na kuwataka waandae mapendekezo ya bajeti kwa kuzingatia taratibu za kiuhandisi na ujenzi na makisio ya awali yalikuwa sh. bilioni 1.3/-.
Alisema alipeleka barua kuomba michango kwa watu binafsi, mashirika ya umma, taasisi, mabenki na balozi mbalimbali ambao hadi sasa wamekwishamchangia sh. milioni 785 na dola za Marekani 267,834 na kwamba hadi sasa kwenye akaunti ya ujenzi amebakiza kiasi cha sh. milioni 40 na dola za Marekani 117,495.

“Katika kuanza zoezi la kukusanya fedha Aprili 2013, Ubalozi wa China ulikuwa wa kwanza kuitikia maombi yetu na ulitoa Dola za Marekani 200,000 ambazo zilikuwa sawa na sh. milioni 320. Pia ubalozi ukamteua mkandarasi wa barabara ya kutoka Nkasi – Kibaoni – Mpanda asaidie katika ujenzi wa shule ili kupunguza gharama,” alisema.

Hadi sasa majengo yaliyokamilika ni madarasa 14, jengo la utawala lenye ofisi za walimu na maktaba mbili (wanafunzi na walimu), jengo la TEHAMA la wanafunzi lenye darasa moja, ukumbi mdogo na ofisi ya mwalimu na majengo mawili ya vyoo yenye matundu 48. Pia ujenzi wa nyumba sita za walimu uko kwenye hatua za mwisho. Nyumba hizo zinajengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Waziri Mkuu aliwaomba watanzania watakaoguswa na jambo hili wamsaidie kutimiza ndoto yake kwani bado anakabiliwa na kazi ya kuweka umeme, maji, kujenga nyumba 18 za walimu, bwalo na jiko, karakana nne za ufundi, vitabu na TABLETS za wanafunzi, kituo cha walimu cha mafunzo ya muda mfupi na utunzaji taarifa (Resource Centre), viwanja vya michezo vya kisasa vinavyozingatia michezo yote, mfumo wa uvunaji maji ya mvua, mfumo wa maji safi na maji taka, nyumba mbili za walinzi na uzio wa shule.

Alitaja vitu vingine ambavyo bado vinahitaji kuchangiwa ni meza za walimu – za ofisini na darasani, viti vya walimu – vya ofisini na darasani, madawati ya shule ya msingi na ya awali, meza na viti vya maktaba zote mbili, meza na viti vya bwalo – shule ya msingi na shule ya awali. Vyote hivi alisema vitagharimu sh. bilioni 2.18.