Jumanne , 24th Feb , 2015

Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda leo ameongoza uzinduzi wa zoezi la uandikishwaji wapiga kura kwenye daftari la kudumu la wapiga kura kwa mfumo wa BVR lililoanza mkoani Njombe

Mwenyekiti wa NEC Jaji mstaafu Damian Lubuva

Jumla ya watu 3014 wakazi wa mji wa Makambako mkoani Njombe wameandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga katika zoezi lililofanyika jana.

Akitoa taarifa hiyo katika uzinduzi rasmi wa zoezi hilo uliofanyika leo mjini Makambako mkoani Njombe, mwenyekiti wa tume ya Uchaguzi Jaji Mstaafu Damian Lubuva ambaye amesema kuwa tume hiyo ilikuwa na matarajio ya kuandisha watu 1850 katika mji huo, lakini imefanikiwa kuandikisha watu 3014.

Amesema zoezi hilo limeanza katika kata 9 za mji wa Makambako ambapo kwa jana jumla ya vituo 54 viliendesha zoezi hilo kwa mafanikio.

Jaji Lubuva amesema hiyo ni ishara kwamba zoezi hilo limeanza kwa mafanikio makubwa tofauti na ambavyo imeripotiwa katika vyombo mbalimbali vya habari kuwa zoezi hilo limeanza kwa kusuasua.

"Kama tulipanga kuandikisha watu 1850 lakini tumeweza kuandikisha watu 3014 hayo siyo mafanikio?? ninyi wenyewe mtakuwa majaji wa kutoa hukumu isiyokuwa na rufaa."

Akizungumzia baadhi ya kasoro zilizojitokeza hapo jana, Jaji Lubuva amesema kuwa suala la baadhi ya vidole vya watu kushindwa kutambuliwa katika mashine za BVR limeshughulikiwa na halitajitokeza tena.

“Tunatakiwa kuwapongeza watu wa Njombe maana inonesha ni jinsi gani walivyo wachapakazi hususani katika mashamba ya chai jambo linalosababisha mikono yao kuwa vile (Sugu)”

Kuhusu kuwepo kwa foleni ndefu, amesema kuwa suala la foleni ni la kawaida kulingana na asili ya kazi yenyewe.

Jaji Lubuva ameonya wanasiasa kutumia mchakato huo kama fursa ya kujipatia umaarufu kwa kuwakatisha wananchi tamaa kuwa zoezi hili haliwezekani.

Kwa upande wake mgeni rasmi katika uzinduzi huo Mh Mizengo Pinda ameelezea umuhimu wa zoezi hilo na kwamba daftari hilo ndilo litakalotumika kwenye upigaji kura ya Maoni kwa ajili ya Katiba Mpya.